Quantcast
Channel: CHIMBUKO LETU
Viewing all articles
Browse latest Browse all 911

NAIBU WAZIRI WA AFYA AENDELEA KUITAMBULISHA PROGRAMU YA ‘KIKUNDI MLEZI’

$
0
0



Naibu Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Faustine Ndugulile ameendelea kuitambulisha programu ya ‘Kikundi Mlezi’ yenye lengo la kuwawezesha wanawake wajasilimali kuwa na mfumo wa kuwezeshana wao wenyewe katika kuanzisha na kuendeleza miradi ya biashara.

Dkt. Ndugulile ameitambulisha programu hiyo wakati alipofanya ziara Wilayani Kigoma Ujiji mkoani Kigoma katika zoezi la kuamsha ari ya wananchi kushiriki ipasavyo katika shughuli za maendeleo katika maeneo yao.

Dkt.Ndugulile amesema kuwa ili kufanikisha kufikia Tanzania ya viwanda Serikali itaendelea kuwasaidia wajasiliamali wadogo wadogo hasa wanawake katika kuwawezesha kuanzisha vikundi vitakayopanua uanzishaji wa viwanda vidogo vidogo na vya kati.

Ameongeza kuwa lengo la kuzindua na kuendeleza Programu ya ‘Kikundi Mlezi’ ni kuwashirikisha wanawake wajasilimali waliokomaa katika biashara kuwasaidia wanawake wajasiliamali wanaoanza shughuli za biashara ili kusisimua ukuaji wa uchumi na wa viwanda.

“Niseme programu hii niliyoizindua Wilayani Kiisarawe itaendelea kusaidia kwa asilimia kubwa kuibua wanawake ambao hawakuwa na uwezo katika kuanzisha biashara zao na kufanya wanawake kujiunga na vikundi na hatimaye kuanzisha viwanda vidogo na vya kati”alisisitiza Mhe. Dkt. Ndugulile.

Kwa upande wake Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Kigoma Dkt. Paul Chaote amesema kuwa programu ya Kikundi Mlezi itasaidia kuwainua wanawake na kujitokeza kwa wingi kujishughulisha na shughuli za uzalishaji ili kufikia azma kuwa na viwanda 100 kwa kila mkoa hapa nchini.

“Tutaendelea kushirikiana na Wizara kuhamasisha wanawake kujitokeza na kujiunga na vikundi na kusaidiana katika kuendesha biashara ambazo zitawasaidia kujikwamua kiuchumi”. Alisisitiza Dkt. Chaote.

Mmoja wa wanawake wajasiliamali Wilayani Kigoma Ujiji Bi. Sophia Ibrahim ameishukuru Serikali kwa kuzindua Mpango huo utakaowawezesha wanawake kusaidiana katika kuanzisha na kuchochea ukuaji wa vipato vyao kutokana na kujenga mfumo wa wanawake kusaidia kujikwamua kiuchumi.

Naibu Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile amefanya ziara ya siku mbili mkoani Kigoma na kuwatembelea wanawake wajasiliamali katika kuhamasisha wanawake kujishughulisha na miradi ili kusaidia kufikia azma ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kuwa na Tanzania ya Viwanda.

Source:- Bongo5

Viewing all articles
Browse latest Browse all 911

Trending Articles